﻿Zaburi.
93.
Bwana anatawala, amejivika utukufu; Bwana amejivika utukufu tena amejivika nguvu. Dunia imewekwa imara, haitaondoshwa. 
Kiti chako cha enzi kimekuwa thabiti tangu zamani; wewe umekuwako tangu milele. 
Bahari zimeinua, Ee Bwana, bahari zimeinua sauti zake; bahari zimeinua sauti za mawimbi yake. 
Yeye ni mkuu kuliko ngurumo ya maji makuu, ni mkuu kuliko mawimbi ya bahari: Bwana aishiye juu sana ni mkuu. 
Ee Bwana, sheria zako ni imara; utakatifu umepamba nyumba yako pasipo mwisho. 
