﻿Zaburi.
3.
Yahewh, maadui zangu wako wangapi! Ni wengi wamekuja kinyume na mimi. 
Ni wengi wanaonisema, “Hakuna msaada wowote kutoka kwa Mungu kwa ajili yake.” Selah 
Bali wewe, Yahweh, u ngao yangu pande zote, utukufu wangu, na uniinuaye kichwa changu. 
Nampazia Yahweh sauti yangu, na yeye ananijibu kutoka katika mlima wake mtakatifu. 
Nilijilaza chini na kusinzia; na niliamka, kwa kuwa Yahweh alinilinda. 
Sitaogopa kusanyiko la watu ambao wamejipanga kinyume na mimi pande zote. 
Inuka, Yahweh! Uniokoe, Mungu wangu! Kwa kuwa utawapiga maadui zangu wote kwenye taya zao; utayavunja meno ya waovu. 
Wokovu unatoka kwa Yahweh. Baraka zako ziwe juu ya watu wako. 
