﻿Zaburi.
54.
Uniokoe, Mungu, kwa jina lako, na kwa nguvu zako unihukumu. 
Usikie maombi yangu, Mungu; uyategee sikio maneno ya mdomo wangu. 
Kwa maana wageni wameinuka dhidi yangu, na watu wasio na huruma wanaitafuta roho yangu; nao hawakumuweka Mungu mbele yao. Selah 
Tazama, Mungu ni msaidizi wangu; Bwana ndiye anisaidiaye. 
Naye atawalipizia uovu maadui zangu; katika uaminifu wako, uwaharibu! 
Nitakutolea dhabihu kwa moyo mkunjufu; nitalishukuru jina lako, Yahwe, kwa maana ni jema. 
Kwa kuwa yeye ameniokoa katika kila shida; macho yangu yamewatazama adui zangu yakiwa na ushindi. 
