﻿Zaburi.
64.
Sikia sauti yangu, Mungu, usikilize malalamiko yangu; unilinde dhidi ya hofu ya adui zangu. 
Unifiche dhidi ya mipango ya siri ya wafanyao maovu, unifiche dhidi ya watendao vurugu ya udhalimu. 
Wao wamenoa ndimi zao kama panga; wamelenga mishale yao, maneno machungu, 
ili kwamba waweze kupiga kutoka mahali pa siri kwenda kwa mtu asiye na hatia; wampige yeye kwa ghafla nao wasihofu lolote. 
Wao wanahamasishana wenyewe katika kupanga uovu; wanashauriana pamoja wao binafsi ili kuweka mitego; nao husema, “Ni nani atakayetuona?” 
Wanabuni mipango ya dhambi; “Tumemaliza,” wanasema, “ni mpango makini.” Mawazo ya ndani na mioyo ya watu ni ya kina. 
Lakini Mungu atawapiga wao; ghafla watajeruhiwa kwa mishale yake. 
Watafanywa kuwa mashakani, kwa kuwa ndimi zao wenyewe ziko kinyume nao; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao. 
Watu wote wataogopa na kutangaza matendo ya Mungu. Kwa hekima watafikiria kuhusu kile yeye ametenda. 
Wenye haki watakuwa na furaha kuhusu Yahwe nao watakimbilia kwake; wote wenye haki moyoni watajivuna katika yeye. 
