﻿Zaburi.
112.
Msifuni Yahwe. Amebarikiwa mtu yule anaye mtii Yahwe, apendezwaye sana na amri zake. 
Kizazi chake kitakuwa ni chenye nguvu duniani; kizazi cha mcha Mungu kitabarikiwa. 
Nyumbani mwake mna utajiri na mali; na haki yake itadumu milele. 
Nuru huangazia gizani kwa ajili ya mtu mcha Mungu; yeye ni wa fadhili, huruma, na haki. 
Heri atendaye fadhili na kukopesha, afanyaye mambo yake kwa uaminifu. 
Kwa maana hataondoshwa kamwe; mwenye haki atakumbukwa milele. 
Haogopi habari mbaya; ni jasiri, akimtumainia Yahwe. 
Moyo wake ni mtulivu, hana woga, mpaka aonapo ushindi dhidi ya watesi wake. 
Huwapa masikini kwa ukarimu; haki yake yadumu milele; atainuliwa kwa heshima. 
Mtu mwovu ataona haya na kukasirika; atasaga meno yake na kuyeyuka; tamaa ya wasio haki itapotea. 
